
Kocha wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre akiongea na kocha wake wa viungo enzi wakiwa Simba.
RASMI
sasa Kocha wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, ametimuliwa Msimbazi.
Hii ni baada ya Mkalimangi kunasa taarifa hizo takriban wiki mbili
kabla.
Lechantre, ambaye alitua Simba Januari, mwaka huu
na kuanza mechi yake ya kwanza Januari 28, ametimuliwa baada ya
kuiongoza Simba kwa mechi 15 tu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kikosi cha timu ya Simba.
Kisa
kikubwa cha kutimuliwa kama ilivyoandikwa katika gazeti bora la michezo
Tanzania, Mkalimangi, ni madai yake ya mshahara wa Sh milioni 90 kila
mwezi ili asaini mkataba mpya.
Pamoja na sababu
hiyo, Lechantre ambaye alikwenda Kenya kuiongoza Simba katika michuano
ya SportPesa Super Cup, jana kabla ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya
Kakamega Home Boys, kocha huyo aligoma kuiongoza timu akidai mkataba
mpya.
Taarifa ambazo Mkalimangi lilikuwa nazo ni kwamba,
Lechantre aliondoka Bongo akiwa amekubaliana na mwekezaji wa Simba,
Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwa atapewa mkataba baada ya kumalizika kwa michuano
ya SportPesa Super Cup.
Lakini jana, alipomuona
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alimlalamikia kuwa hana
mkataba na akadai hawezi kuendelea kuiongoza timu hiyo akiwa hana
mkataba.
Baada ya mabishano ya muda mrefu, Try
Again alikubali kwamba asiiongoze Simba jana dhidi ya Kakamega, na
badala yake Mfaransa huyo akaenda kukaa jukwaani na mashabiki akiwa
amenuna, huku msaidizi wake Masoud Djuma akiiongoza Simba kutinga
fainali kwa mikwaju ya penalty 5-4
Baada ya kugoma
kuiongoza timu hiyo jana, ndipo ikaelezwa kuwa Try Again akachukua
uamuzi wa kumng’oa rasmi Mfaransa huyo ambaye ameiongoza Simba kubeba
ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, akichukua mikoba ya
Mcameroon, Joseph Omog ambaye alimaliza mzunguko wa kwanza akiwa
hajapoteza mechi yoyote.
Mkalimangi linafahamu kuwa
Mfaransa huyo asingeweza kuendelea kuwa kocha wa Simba kutokana na
Wekundu hao kukerwa na tabia yake ya kupenda fedha kupita kiasi, huku
pia wakiwa hawafurahishwi na aina ya soka lake.
Simba
pia ilikerwa na namna kocha huyo alivyowatumia wachezaji wake, wengine
akiwachezesha katika nafasi zisizo zao, mfano straika Nicholaus Gyan
ambaye alikuwa anachezeshwa kama beki wa pembeni chini ya Lechantre.
Hata
hivyo, Mkalimangi linafahamu kuwa Simba pia haikuwa ikipendezwa na
misimamo ya kocha huyo ambaye alikuwa hataki kuingiliwa katika mipango
yake ya kikosi.
Mkalimangi lilimpata Kaimu Rais wa Simba, Try
Again, jana mchana akathibitisha kuwa kocha huyo anaondoka lakini
akakataa kufafanua zaidi akidai atazungumza mengi kuhusu ufafanuzi huo
baadaye.
“Akitoka hapa, kocha atakwenda kwao, kuna
matatizo yametokea. Kwa sasa siwezi kuyaeleza kwa kirefu, nitayatolea
ufafanuzi baada ya harakati hizi,” alisema Try Again.
Wachezaji
wa Simba, jana walishtushwa kutokana na kutokumuona kocha wao katika
benchi la ufundi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya Kakamega
Home Boys.
Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima,
alisema baada ya kushinda mechi ya jana na kutinga fainali, wachezaji wa
timu hiyo walikwenda jukwaani kushangilia na Lechantre ili kumpa
heshima yake kutokana na mchango wake katika Klabu ya Simba.
“Tulikwenda
kushangilia kwa kocha kama kumuonyesha heshima, matatizo yao na uongozi
hayatuhusu, maana tuliuliza kwa nini hayupo, tukaambiwa mwenye macho
haambiwi tazama,” alisema Niyonzima.
Lechantre
anaondoka Simba akiwa ameshinda mechi 10, ikiwemo dhidi ya mahasimu wao,
Yanga huku akiwa ametoa sare nne na kufungwa mechi moja katika Ligi Kuu
Bara.
Msaidizi wake, Mtunisia, Aimen Mohammed
Habib, atafuatana naye kuondoka Simba, kwani naye jana aligoma kuiongoza
Simba dhidi ya Kakamega
Simba itaendelea kuwa na Djuma kama kocha mkuu huku ikiendelea kusaka kocha wa kuvaa viatu vya Lechantre
Post a Comment